Kituo Cha Fursa
Elimu ya Maendeleo ya Wananchi ni elimu inayotolewa kwa mwananchi ili kumuwezesha kupata maarifa, ujuzi na umahiri katika matumizi ya rasilimali zilizopo na kutawala mazingira ili kuleta maendeleo ya haraka kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Elimu hii inatolewa katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kupitia mfumo rasmi na mfumo usio rasmi kulingana na mahitaji ya mwananchi.
Kuwa Chuo kinachoongoza katika utoaji wa ujuzi kulingana na mahitaji ya jamii nchini na Afrika Mashariki.
Kusimamia na kushauri kuhusu utoaji wa ujuzi kulingana na mahitaji ya jamii kwa kutumia mitaala husika, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi kwa wadau.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Bigwa (CMW Bigwa) ni miongoni mwa vyuo hamsini na nne, vilivyo anzishwa mwaka 1975 kutokana na wazo la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere, baada ya kutembelea nchi ya Sweden na kuona mfumo wa elimu isiyokuwa rasmi ulivyokuwa unaendeshwa na taasisi zinazojulikana kama Folk High Schools.
Kilianzishwa kama sehemu ya awamu ya tatu ya Elimu ya Watu Wazima. Hatua ya kwanza ilihusu kuondoa ujinga wa kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu. Hatua ya pili ilikuwa ya kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyopatikana katika hatua ya kwanza yanakuwa endelevu na watu hawaurudii ujinga. Hatua ya tatu ilikuwa kuanzisha taasisi ambazo zingetoa maarifa na stadi kwa wananchi. Aidha, uamuzi wa kuanzishwa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ikiwemo CMW Bigwa ulitokana na Waraka wa Baraza la Mawaziri No. 96 wa mwaka 1974 ambapo vyuo 25 vilianzishwa mwaka 1975 na kuendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kulingana na jinsi Wilaya mbalimbali zilivyo tambua umuhimu wa kuanzisha vyuo hivi. Hadi kufikia mwaka 1978, vyuo 53 vilikuwa vimeanzishwa.
Uanzishwaji wa VMW ulizingatiwa katika Sheria ya Elimu No. 25 ya mwaka 1978 chini ya Wizara ya Elimu. Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilipoanzishwa vilirithi majengo yaliyokuwa yakitumika kwa madhumuni tofauti tofauti vikiwemo Vituo vya Mafunzo ya Maendeleo Vijijini (Rural Training Centres) ambavyo vilianzishwa mwaka 1962, Vituo vya Mafunzo ya Wakulima (Farmers Training Centres) ambavyo vilianzishwa mwaka 1963, Shule za Kati (Middle Schools) ambazo zilianzishwa mwaka 1960 na Vituo vya Mafunzo ya Ushirika vilivyoanzishwa mwaka 1964. Vyuo pekee vilivyojengwa mahsusi kuitikia wazo la Baba wa Taifa la mwaka 1975 ni vinne, vyuo hivyo ni Sengerema, Ngara, Handeni na Bigwa, ambavyo vilijengwa mwaka 1975.